Masharti ya matumizi

Imesasishwa mwisho 4 Oktoba 2026

Masharti haya ni makubaliano kati yako na Fika. Tafadhali yasome: kwa kufungua akaunti au kutumia Fika unayakubali.

  1. 1.Fika ni nini

    Fika hukusaidia kuandaa tukio: unatunza orodha ya wageni, unamtumia kila mgeni mwaliko kwa WhatsApp au SMS, unarekodi ahadi na malipo, na kuwakumbusha wageni kuhusu ahadi zao.

    Anayeunda tukio ndiye mwandaaji wake. Masharti haya yanawahusu waandaaji na yeyote anayetembelea Fika.

  2. 2.Akaunti yako

    Unahitaji akaunti ili kuandaa tukio. Toa barua pepe halisi na utunze nenosiri lako. Unawajibika kwa yanayofanyika kupitia akaunti yako.

    Lazima uwe na umri wa miaka 18 au zaidi ili kufungua akaunti.

  3. 3.Wageni wako na ujumbe wako

    Unaongeza mwenyewe majina na namba za simu za wageni wako. Kwa kuwaongeza, unathibitisha kuwa unaruhusiwa kuwasiliana nao kuhusu tukio lako.

    Mialiko na vikumbusho hutumwa kwa jina lako, kwa watu uliowaalika. Huruhusiwi kutumia Fika kutuma matangazo, ujumbe usiotakiwa, au chochote kilicho kinyume cha sheria, cha vitisho au cha kupotosha.

    Unawajibika kwa taarifa za tukio lako na kwa yaliyomo kwenye ujumbe wako.

  4. 4.Nafasi za kutuma na malipo

    Kutuma mialiko na vikumbusho vya ahadi hulipiwa kwa nafasi za kutuma, unazonunua kwa pesa za simu. Bei huonyeshwa kabla ya kulipa.

    Nafasi moja ya mwaliko hutoa kadi moja ya WhatsApp na SMS moja kwa tukio hilo. Kumtumia tena mgeni yuleyule hutumia nafasi nyingine. Ujumbe ulioshindikana hautozwi.

    Muundo wa kadi wa tukio huchaguliwa kwenye malipo ya kwanza na hauwezi kubadilishwa baadaye.

    Nafasi zilizokwisha tumika hazirejeshewi pesa. Kama malipo yamekosea, kwa mfano umetozwa na nafasi hazikuongezwa, wasiliana nasi na tutalifuatilia.

  5. 5.Ahadi na michango

    Fika hurekodi ahadi na malipo unayoyaingiza. Pesa zenyewe hutoka kwa wageni wako moja kwa moja kwenda kwenye namba za simu au akaunti za benki unazowapa. Fika haipokei, haitunzi wala haipitishi pesa hizo, na si sehemu ya makubaliano hayo.

  6. 6.Kufika kwa ujumbe

    Ujumbe hupita kwenye WhatsApp na mitandao ya simu, ambayo Fika haiidhibiti. Tunakuonyesha ujumbe uliotumwa na ulioshindikana, lakini hatuwezi kuahidi kuwa kila ujumbe utamfikia mgeni au kusomwa.

  7. 7.Miundo ya kadi na jina la Fika

    Miundo ya kadi, jina na nembo ya Fika, na tovuti ni mali ya Fika. Unaweza kutumia miundo kwa matukio yako ndani ya Fika. Huruhusiwi kuinakili, kuiuza au kuitumia mahali pengine.

  8. 8.Kufunga au kusimamisha akaunti

    Unaweza kuacha kutumia Fika wakati wowote na kufuta matukio yako. Tunaweza kusimamisha au kufunga akaunti inayovunja masharti haya, inayodhuru watu wengine, au inayotumika kwa udanganyifu.

  9. 9.Wajibu wetu

    Tunajitahidi Fika ipatikane na iwe sahihi, lakini inatolewa kama ilivyo. Kwa kadiri sheria inavyoruhusu, Fika haiwajibiki kwa hasara zisizo za moja kwa moja, kama mgeni aliyekosa mwaliko, ujumbe uliochelewa au tukio lisiloenda kama lilivyopangwa.

  10. 10.Mabadiliko ya masharti haya

    Tunaweza kusasisha masharti haya. Tarehe iliyo juu huonyesha toleo la karibuni. Ukiendelea kutumia Fika baada ya mabadiliko, unakubali masharti mapya.

  11. 11.Sheria inayotumika

    Masharti haya yanaongozwa na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

  12. 12.Wasiliana nasi

    Una swali kuhusu ukurasa huu? Wasiliana na timu ya Fika.